Nyumbani imesikika,
Mlango ukapigika,
Kelele kubwa metoka,
Mjumbe ameshafika,
Machozi yatiririka,
Moyo umeshavunjika,
Loo! Baba Mwanjonde katoka.
Baba Mwanjonde katoka,
Kenda kwa alompeleka,
Alofanya kaumbika,
Ni huzuni kwa hakika,
Kwake Mungu atapumzika,
Imani yetu kafika,
Kweli hatuna mashaka,
Bwana ndiye kamtaka.
Bwana ndiye kamtaka,
Alotufanya kucheka,
Kwa upole alipendeka,
Utume alisifika,
Baridi imekushika,
Joto kwako limetoka,
Mtu mwema kaondoka,
Mwanjonde ametutoka.
Mwanjonde ametutoka,
Ulimi umekauka,
Kwa tenzi tunatenzika,
Huzuni na hekaheka,
Ni wazi na ni hakika,
Nasi huko tutafika,
Padre Timothy nenda,
Nenda salama Mwanjonde.
Hatuna cha kulaumu,
Mungu kwake ziwe sifa,
Sote tulo binadamu,
Ni hakika tutakufa,
Hakuna sintofahamu,
Mwanjonde metangulia,
Na kesho tutamfuata.
Kwaheri Baba
Kwaheri Sana Baba
Safari umemaliza Baba
Lala salama Baba
Nasi baadayi tutakufuata Baba.