Eti,vijana leo siyo yenu ngojeni kesho! Hahahaha...
Msemo huu hauna tofauti na ule usemao “Vijana ni taifa la kesho”! Mnanitia uvivu
kutumia nguvu, akili na vipaji vyangu kufanikisha mambo kwa kuingojea kesho yenu
isiyofika. Hivi kesho ilishawahikufika? Na ikishafika Inaitwaje? Ikikaribia
haiitwi tena kesho hiyo ni leo, ndiyo sasa. Na siku ile uliyoitumia kusema
kesho itaitwa jana. Kesho iko wapi? …haaaaaa!.. ndiyo ile imeitwa jana au ndiyo
hii inaitwa leo? Wewe kesho, mbona hufiki? Kumbe jana ni halisi na leo pia ni halisi
kwamaana jana imepita na leo ndiyo sasa, lakini kesho haijafika. Hakika kesho haijawahi
fika, kesho haijawahi kuwa, inabaki akilini tu. Kesho uniache, mimi najituma sasa.
Utasikia mmoja anasema, ndugu yangu nivumilie kidogo
kesho nitakupatia mzigo wako; na mwingine anasema, rafiki kesho nitakutumia pesa
kidogo. Hizi ni baadhi ya kauli za kuleta matumaini kuifikia kesho japo haifikiki.
Atakapokupatia mzigo wako siyo tena kesho bali ni leo; akikutumia pesa siyo tena kesho bali ni sasa.
Kesho itaendelea kubaki kwenye akili na siyo kwenye uhalisia. Nifupishe tu maneno, kwamba
kesho haifiki daima. Hata uwe na mbio kiasi gani huwezi kuifikia kesho, na hata
uwe mrefu wa futi nane kama Robert Wadlow huwezi kuiona kesho. Labda wanasayansi
watusaidie ndege za mwendokasi tuikimbize; wenzenu wa Dar-essalaam wana mabasi ya
mwendo kasi lakini mpaka sasa bado hawajaifikia kesho. Labda Flyovers zitawapa matumaini
ya kuifikia kesho.
Falsafa hii ya maisha (vijana taifa la kesho) inanyima
fursa na kudogosha vijana katika bidii za kuleta maendeleo katika jamii. Kauli hii
hufubaisha fikra kwa vijana na kupelekea vijana kungojea kupewa amri na kufanyiwa
vitu vingi bila wao kushiriki kikamilifu au kujituma kikamilifu kwa maana leo siyo
yao wanangoja kesho ambayo haijawahi kufika.
Kauli hii inatoa fursa zaidi kwa wale walio vuka umri
wa ujana (watu wazima) kuwadharauna kuwadogosha vijana katika kutoa mawazo, mapendekezo
na hata kusimamia misimamo yao katika maisha ya kila siku. Nazani ulishawahi kusikia
au kuambiwa “utatuambia nini? Wewe bado kijana sana, subiri ukue ndiyo utoe mawazo,
tusikilize sisi wazee kwanza”. Sitaki kukwambia usiwasikilize wazee bali ninyi mlio
wazee wapeni vijana nafasi ya kutoa mawazo bila kuwabeza kwa kauli za namna hiyo
maana vijana wana fikra motomoto. Ndiyo kusema kwamba, malumbano mengi na misuguano
hasi ya kimawazo kati ya vijana na watu wazima huanzia kwenye falsafa hii ya vijana
taifa la kesho au kusema vijana leo siyo yenu ngojeni kesho.
Mimi niliye kijana ninayesukumwa na moyo wangu kuhitaji
usalama, uhuru, kufaulu, utulivu moyoni na kupata heshima ndiye taifa la sasa, leo
ndiyo yangu kwa maana natambua kwamba kesho haijawahi kufika na hata ikifika siyo
tena kesho na ikipita siyo tena kesho. Vijana muda ni sasa tusingoje kesho...! Tusipumbazwe
na kauli "vijana taifa la kesho" hii itafaa kwa watoto. Nasema tena, achana
na falsafa ya ngoja kesho wewe ni taifa la sasa.
Vijana
leo ndiyo yetu, kesho haifiki.

Nice word
ReplyDelete