Shukrani kwako, Mama mzazi
Mambo yako yanaonekana waziwazi
Umetusafisha na kutuvalisha mavazi
Umetulea na kutufundisha Kazi
Nyumbani Kipalapala, mazuri makazi
Twakushukuru Mama; daima tunasema asante.
Kulea watoto, Mama kweli unaweza
Wimbo mzuri miguuni umetuachia kucheza
Maisha yetu bora, kweli umeyatengeneza
Upendo; Mama umetupatia bila kubakiza
Huu wosia, basi tuende kuutekeleza
Twakushukuru Mama; daima tunasema asante.
Mengi mazuri, kwako tumepata
Njia yako, tunakiri inameremeta
Malezi Safi, mengi tumechota
Tumeishi kweli, bila kujuta
Asante Mungu; Kip umetuleta
Twakushukuru Mama; daima tunasema asante.
Mama basi kwakheri! Tutarudi kukusalimia
Baraka zako; tunajua popote zitatufikia
Baki salama; Imani uendelee kuipalilia
Usiku na mchana, nguvu umetutia
Asante Sana, kutuonyesha hii njia
Twakushukuru Mama; daima tunasema asante.
Basi kwakheri, Mama Kipalapala
Tunakupenda sana, bila hila
Mama asante, umetupatia fadhila
Ukarimu wako, hauna mjadala
Kwakheri Mama, umetusaidia jumla
Twakushukuru Mama; daima tunasema asanteee.

Very good poem in terms of structure and contents.
ReplyDelete